Wazazi na Walezi watakiwa kuelewa dhana ya Elimu bila Malipo
Wazazi na walezi katika Halmashauri ya Mji Geita wamegizwa kuchangia na kushiriki kikamilifu katika kuendesha shule zilizoko katika maeneo yao hususani katika majukumu kama upatikanaji wa chakula shuleni na kushiriki shughuli za ujenzi.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi Teknolojia na ufundi Profesa Simon Msanjila alipokuwa katika ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Geita hivi karibuni.
Profesa Msanjila amefafanua kuwa sehemu kubwa ya wanajamii hawaielewi dhana ya elimu bila malipo iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kudhani kwamba mzazi hana jukumu lolote katika kuhakikisha mazingira ya kufundishia na kujisomea shuleni yanakuwa rafiki kwa mwanafunzi.
“Kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo katika shule za Msingi Wilayani Geita. Hivyo ni jukumu la Halmashauri kwa kushirikiana na makampuni, Taasisi binafsi, wafanyabiashara na wazazi kuchangia katika ujenzi na ukamilishaji wa miundo mbinu hiyo ili kuboresha sekta ya elimu wilayani kwenu. Tambueni kuwa hakuna zawadi kubwa ambayo mzazi/mlezi anaweza kumpa mtoto na asiisahau maishani Zaidi ya Elimu”. Aliongeza Profesa Msanjila.
Katika ziara yake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi Teknolojia na Ufundi alipata fursa ya kutembelea shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu na kukagua jengo la bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum litakaloanza kutumika mwaka 2018 katika Shule ya Msingi Mbugani.
Akiwa katika Shule ya Msingi Mbugani, Profesa Msanjila aliwapongeza walimu wanaofundisha watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali na kukagua nyenzo zinazotumika kuwafundishia wanafunzi hao. Pia aliagiza Halmashauri ya Mji Geita kuandaa andiko litakaloainisha gharama za ujenzi wa jengo la kupima afya za watoto wanaopelekwa shuleni hapo kabla ya kuwapa elimu kulingana na tatizo alilonalo mwanafunzi.
Katika kuhitimisha ziara yake ndani ya Halmashauri ya Mji Geita, Profesa Msanjila alitembelea shule binafsi ya Sekondari ya Wasichana Waja ambapo alikabidhi zawadi ya magari mawili yenye thamani ya Shilingi Milioni 22 yalitolewa na Mmiliki wa shule za Waja kwa wanafunzi Edna Meela na Biera Kabaruka waliomaliza kidato cha sita masomo ya Sayansi katika shule hiyo mwaka 2017 na kufanikiwa kuingia katika orodha ya wanafunzi kumi bora kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa