UKAMILIFU WA JENGO LA UTAWALA KUONDOA KERO YA MSONGAMANO
Imebainishwa kuwa kukamilika kwa jengo kubwa la ghorofa la utawala lenye majengo mawili( two in one) linalojengwa katika eneo la Magogo Kata ya Bombambili, Halmashauri ya Mji wa Geita kutawezesha kuondoa msongamano wa watumishi wa Halmashauri ya Mji Geita ambao kwa sasa wamebanana katika Ofisi ndogo zinazotumika kwa muda.
Kauli hiyo imebainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Modest Apolinary hivi karibuni wakati akipokea jengo hilo kutoka kwa Mkandarasi aliyejenga, baada ya ujenzi kukamilika kwa awamu ya kwanza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita amesema kuwa kutokana na msongamano wa watendaji katika Ofisi zinazotumika hivi sasa kunapunguza ufanisi wa kazi kwani muda mwingine huwalazimu watumishi kukaa kwenye viti kwa zamu. Hivyo jengo hilo litakapokamilika watumishi watapata ari mpya ya kutekeleza majukumu yao.
“Licha ya kutumika kama Ofisi, jengo hilo litakuwa kitega uchumi cha Halmashauri kwa sababu kutakuwa na maeneo yatakayopangishwa kwa Benki mbalimbali pamoja na kuwa na soko dogo la kuuzia dhahabu hivyo kuendelea kufungua fursa za kiuchumi katika Mji wa Geita.” Aliongeza Mhandisi Modest Apolinary.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita, Mhe. Leonard Bugomola amesema kuwa jengo hilo la kisasa litabadili sura ya Mji wa Geita na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kutosimamisha ujenzi wa mradi huo badala yake kasi ya ujenzi iongezwe kwa kutumia mapato ya ndani yatakayokusanywa ili kukamilisha ujenzi mapema
Jengo la kisasa la utawala la Halmashauri ya Mji wa Geita lilianza kujengwa mwaka 2016 umegharimu kiasi cha Shilingi bilioni 2.5 alizolipwa Mkandarasi na Shilingi Milioni 174 kwa msimamizi, litakuwa na vyumba 114 vya Ofisi litawawezesha watu wote kulitumia wakiwemo walemavu ambao wamewekewa njia zao kuanzia mwanzo hadi ghorofani na kila ghorofa kuwa na choo maalum kwa ajili ya walemavu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa