Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, leo amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita Mkoani Geita na kutembelea maeneo ya Nyakabale na Nyamalembo ambapo ametatua rasmi mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 26 kati ya wananchi wa maeneo hayo na Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML).
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Shigela aliwapongeza wananchi wa Nyakabale na Nyamalembo kwa kuvumilia hali hiyo kwa muda mrefu bila kuanzisha vurugu wala maandamano, hali iliyodhihirisha ukomavu na uzalendo wao katika kulinda amani na utulivu wa taifa.
Waziri Mavunde, akizungumza mbele ya wananchi, alieleza kuwa baada ya kupokea taarifa rasmi kutoka kwa Kamati ya Vigingi iliyoandaliwa kwa kushirikiana na Mgodi wa GGML, kampuni hiyo imekubali kulipa fidia kwa wananchi husika kwa mujibu wa taratibu na sheria za nchi.
Aidha, alieleza kuwa baada ya kukamilika kwa ulipaji wa fidia, wananchi wote wa maeneo yaliyotambuliwa watatakiwa kuondoka ili kuupisha mgodi kuendelea na shughuli za uchimbaji katika maeneo hayo.
Waziri alitoa onyo kwa baadhi ya watu wanaojaribu kuanzisha ujenzi wa makusudi (tegesha) kwa lengo la kudai fidia isiyo halali. Alisisitiza kuwa Serikali ina taarifa sahihi na picha za anga za eneo hilo, hivyo hakuna nafasi ya udanganyifu. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na Serikali kuhakikisha zoezi hilo linakwenda kwa haraka na kwa amani.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa