Tarehe 22 Septemba 2025, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alifungua rasmi Maonesho ya 8 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maonesho haya makubwa ambayo yalianza rasmi Septemba 18, 2025, yamewakusanya washiriki zaidi ya 600 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wafanyabiashara, wananchi na wadau wa sekta ya madini. Washiriki hao wanaonesha teknolojia mbalimbali zinazotumika kwenye shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na usafishaji wa madini, huku wakipeana maarifa ya kitaalamu na ya kiufundi.
Akihutubia kwenye ufunguzi huo, Mhe. Majaliwa alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya wadau wa madini na Serikali, akieleza kuwa sekta ya madini ni injini muhimu ya maendeleo ya taifa na inaweza kuleta manufaa makubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo iwapo itaendelezwa kwa weledi, uwazi na uadilifu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela, alitoa salam za mkoa na kueleza kuwa Geita imefanikiwa kutekeleza agizo la awali la Waziri Mkuu, ambalo baadaye lilisisitizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu uimarishaji wa miundombinu ya kudumu katika viwanja vya maonesho hayo,
Aidha, alibainisha mafanikio ya wachimbaji wadogo mkoani Geita, akieleza kuwa mwaka 2021 zilitolewa leseni 900 kwa wachimbaji wadogo, na ndani ya kipindi cha miaka minne, wameweza kuzalisha tani 22,000 za madini, huku migodi mikubwa ikizalisha tani 74, jambo linaloonesha mchango mkubwa wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa elimu, ubunifu na ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali, huku Geita ikithibitisha nafasi yake kama kitovu cha madini nchini Tanzania.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa