Leo Tarehe 27 Oktoba 2025, Halmashauri ya Manispaa ya Geita imefanya hafla ya kuwaaga rasmi walimu 11 waliostaafu kwa heshima kubwa baada ya kulitumikia Taifa kwa muda mrefu kwa uaminifu na kujitolea.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Bi. Ellah Makese, ambaye aliwapongeza walimu hao kwa hatua ya kihistoria waliyoifikia. Katika hotuba yake, Bi. Makese alieleza kuwa wastaafu hao wamekuwa mfano wa kuigwa kwa utumishi wao uliojaa hekima, busara, uvumilivu na uadilifu mkubwa.
“Kupitia ninyi tumefundishwa thamani ya utumishi uliotukuka. Mmeacha alama isiyofutika kwa kazi zenu nzuri,” alisema Bi. Ellah.
Aliwahimiza kuendelea kujitunza, kujipenda na kuishi maisha yenye furaha na afya njema. Pia aliahidi kuwa Halmashauri itaendelea kuwatembelea na kuwatafuta mara kwa mara kwa ajili ya ushauri kutokana na uzoefu wao mkubwa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Bi. Ellah aliwataka watumishi waliobaki kazini kujifunza kupitia hafla hiyo, akisisitiza kuwa huu ni wakati wa kutafakari juu ya wapi walipo na wapi wanakoelekea
“Leo siyo tu siku ya kuagana bali ni somo. Wenzenu wamefikia hatua hii ya heshima kwa sababu ya utumishi wao uliotukuka. Ni wakati wenu sasa kuweka bidii, kuwa waaminifu na kujituma zaidi ili nanyi siku moja mfike hapa mkiwa na heshima kama yao,” aliongeza.
Hafla hiyo ilihusisha burudani, chakula cha pamoja na zawadi kwa wastaafu, ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wao mkubwa katika sekta ya elimu ndani ya Manispaa ya Geita.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa