Geita, 30 Agosti 2025
Katika hali ya furaha na shangwe, watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita pamoja na wananchi wamejitokeza mapema leo kuipokea timu ya wachezaji wa Manispaa ya Geita waliokuwa wakishiriki mashindano ya SHIMISEMITA 2025 yaliyofanyika jijini Tanga.
Mashindano hayo ya kitaifa, yaliyoshirikisha watumishi kutoka Halmashauri mbalimbali nchini, yalianza tarehe 15 Agosti 2025 ana kufikia tamati rasmi mnamo tarehe 29 Agosti 2025. Timu ya Manispaa ya Geita imerejea nyumbani ikiwa imeng’ara kwa ushindi mkubwa katika michezo mbalimbali.
Katika mafanikio yake makubwa, timu ya Geita MC imeshinda kombe la mshindi wa kwanza kwenye mchezo wa Basketball (Wanaume), ikiibuka kuwa bingwa wa taifa kati ya timu zote zilizoshiriki. Vilevile, timu ya Volleyball (Wanawake) imejinyakulia nafasi ya tatu kitaifa.
Mbali na ushindi huo mkubwa, timu ya Geita MC pia ilifanya vizuri kwenye michezo mingine ambapo katika mchezo wa Bao na Karata ilishika nafasi ya nne.
Akizungumza wakati wa mapokezi, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Geita, Bi. Ngianasia Kisamo, aliwapongeza wachezaji kwa kuonyesha bidii, nidhamu na ari kubwa ya ushindani katika mashindano hayo.
“Ninawapongeza sana kwa ushiriki wenu mzuri na kwa kuiletea heshima Manispaa ya Geita. Mmeonyesha kuwa tuna vipaji na tunaweza tukipewa nafasi. Kama ofisi, tutaendelea kutoa ushirikiano na kuimarisha timu za michezo kwa watumishi wetu,” alisema Bi. Ngianasia.
Hata hivyo Wachezaji Wamemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndugu Yefred Myenzi kwanamna alivyo wawezesha kwani wameishi kwa tabasamu katika kipindi chote walipokuwa Tanga katika mashindano hayo.
Mapokezi hayo yaliambatana na shamrashamra mbalimbali kutoka kwa wananchi walioguswa na mafanikio ya timu hiyo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza michezo kama sehemu ya kujenga mshikamano na afya miongoni mwa watumishi wa umma.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa