Sekondari Mpya Shiloleli Kuwakomboa Wanafunzi
Kukamilika kwa ujenzi wa Shule mpya ya kwanza ya Sekondari katika kata ya Shiloleli Halmashauri ya Mji wa Geita ambayo inajengwa kupitia mradi wa SEQUIP kutoka Serikali kuu kutawatatulia changamoto ya kutembea umbali wa kilomita 16 kwa safari moja wanafunzi wa kata hiyo ambao kwa sasa wanakwenda kupata masomo yao katika Shule ya Sekondari Bulela iliyoko kata ya Jirani.
Akizungumza na mwandishi wa Habari hii hivi karibuni, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bulela Mwalimu Pelicia Ponsian ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwakumbuka wanafunzi wa Shiloleli na kuona umuhimu wa kupata shule katika mazingira yao.
Mwalimu Ponsian amesema kuwa uwepo wa shule hiyo mpya utawasaidia jumla ya wanafunzi 183 wanaosoma katika shule yake wanaotoka kata ya Shiloleli ambapo wanatembea umbali mrefu na wakati mwingine hususan kipindi cha masika wanakwama kufika shuleni au kufika shule kwa kuchelewa na kukuta masomo yameshaanza kufundishwa.
Mwalimu Ponsian ameongeza kuwa changamoto nyingine ni matokeo ya wanafunzi hao yamekuwa si ya kuridhisha kwa sababu uelewa wao darasani hupungua kutokana na uchovu wa safari ya kutoka nyumbani hadi shule, kushinda njaa, utoro wa rejareja ambao husababishwa na sababu zilizo nje ya uwezo wa wanafunzi kama uwepo wa wanyama wakali na vibaka kwenye mapori wakati wa kwenda shuleni.
Mayala Samike, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Bulela ni miongoni mwa wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kufika shuleni, ambaye amesema kushinda na njaa Pamoja na kukosa vipindi vya kwanza darasani imekuwa sehemu ya Maisha yao hali inayopelekea kuzorota kwa uwezo wake kitaaluma kwani wakirejea nyumbani baada ya masomo wanakuwa na uchovu ambao huwalazimu kulala na kushindwa kupata muda wa kujisomea shuleni.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Shiloleli Mhe. Boniphace Kaswahili Fulano amesema yeye ameunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa bure eneo lake lenye Zaidi ya ekari tisa ili shule ya Sekondari ya kwanza iweze kujengwa na kuwanufaisha Watoto wa kata hiyo. Pia ametoa wito kwa wazazi kuwahamasisha Watoto kupenda shule kwani elimu ndiyo ufunguo wa Maisha.
Shule mpya ya Sekondari katika Kata ya Shiloleli ni miongoni mwa shule mpya 11 za Sekondari zilizojengwa katika Halmashauri ya Mji Geita kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufika shule kwa baadhi ya wanafunzi wanaotumia muda mwingi kutembea mpaka shuleni kwa ajili ya masomo.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa