Leo tarehe 24 Novemba 2025, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba, ameongoza kikao kazi maalum kilichowakutanisha Maafisa Kilimo na Mifugo kutoka kata zote 50 za Wilaya ya Geita. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa EPZ Bombambili na kuhudhuriwa pia na wataalamu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Geita.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Komba amezitaka Halmashauri ya Manispaa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuwekeza kwa nguvu katika sekta kuu tatu za uzalishaji – Kilimo, Ufugaji na Uvuvi – ambazo tayari zimechangia zaidi ya Shilingi bilioni moja katika mapato ya Wilaya.
Katika kuhakikisha sekta hizi zinatoa matokeo zaidi, Mhe. Komba ametoa maagizo matatu muhimu:
1. Pembejeo kwa Bei Elekezi
Amesisitiza kuwa maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuongeza tija katika sekta ya kilimo. Hivyo, wauzaji wa pembejeo wanapaswa kuzingatia bei elekezi na kuhakikisha pembejeo hizo zinawafikia wakulima kwa wakati.
2. Maafisa Kilimo Kata Kuwafuata
Amewataka Maafisa Kilimo wa Kata kuwafuata wakulima mashambani na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili kwa ukaribu na kwa wakati.
3. Ramani Maalum ya Kilimo Geita
Ameelekeza kuandaliwa kwa ramani maalum ya kilimo itakayobainisha mazao yanayostawi kulingana na mazingira ya kila eneo, ili kusaidia kupanga kwa ufanisi aina ya mazao kulingana na maeneo.
Aidha, kwa upande wa sekta ya mifugo, Mkuu wa Wilaya amewaagiza Maafisa Mifugo kuhakikisha wanadhibiti wizi wa mifugo kwa kuhakikisha kila mnyama anayesafirishwa kutoka eneo moja kwenda jingine anakuwa na kibali halali cha serikali.
Mhe. Komba ameahidi kuwa balozi wa sekta hizo kwa kushirikiana na wakulima na wafugaji katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ili kuimarisha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa