Usiku wa tarehe 26 Septemba 2025, Kampuni ya GF Trucks & Equipment Ltd, inayojihusisha na shughuli mbalimbali za usambazaji wa magari na vifaa vizito vya kiufundi, iliandaa tukio maalum la kuwakutanisha wadau wake waliokuwa bega kwa bega nayo kwa muda mrefu. Tukio hilo lilipewa jina la “GF Day” na lilifanyika kwa lengo la kushukuru, kuthamini, na kuimarisha mahusiano ya kibiashara na wadau wake muhimu kutoka sekta mbalimbali.
Hafla hiyo iliambatana na utoaji wa tuzo maalum kwa taasisi na mashirika yaliyoshirikiana kwa karibu na kampuni hiyo. Miongoni mwa waliotunukiwa tuzo hiyo ni Halmashauri ya Manispaa ya Geita, ambayo imetambuliwa kwa kuwa mdau wa kipekee na mshirika wa muda mrefu wa kampuni hiyo. Tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Ndugu Yefred Myenzi.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Myenzi alieleza kuwa kampuni ya GF Trucks ni miongoni mwa taasisi binafsi zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa wa Geita. Aliwahamasisha kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuwekeza zaidi katika sekta muhimu kama afya, elimu, miundombinu, na huduma za kijamii, kwa manufaa ya wananchi wa Geita na Taifa kwa ujumla.
GF Trucks kupitia hafla hii imeonesha dhamira yake ya dhati ya kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo na mdau muhimu katika ustawi wa jamii.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa