Katika kuendeleza heshima na kuthamini mchango wa walimu waliolitumikia Taifa kwa uaminifu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Ndugu Yefred Myenzi, alishiriki kikamilifu katika hafla ya kuwaaga walimu 11 waliostaafu rasmi, hafla iliyofanyika tarehe 27 Oktoba 2025.
Akiwa miongoni mwa wageni wa heshima, Mkurugenzi Myenzi alikabidhi vyeti vya kutambua mchango wao, pamoja na zawadi mbalimbali kwa wastaafu na walimu waliotambuliwa kwa namna ya kipekee.
Katika hotuba yake fupi lakini yenye kugusa hisia, Mkurugenzi Myenzi aliwapongeza wastaafu hao kwa kufika hatua ya heshima, akisisitiza kuwa siyo jambo dogo kwa mtumishi kustahimili changamoto za utumishi hadi kufikia kustaafu akiwa na afya njema.
“Kufika hatua hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini pia ni matokeo ya uadilifu wenu, nidhamu na bidii ya kazi,” alisema Myenzi.
Aidha, aliwatakia maisha mema, afya njema na mafanikio katika majukumu yao ya kibinafsi baada ya utumishi wa umma. Alisisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kuwaheshimu na kuwathamini kwa kuwa wao ni hazina ya hekima na uzoefu mkubwa
Kwa upande wa watumishi waliobaki, Mkurugenzi aliwataka kuendeleza moyo wa kujituma, uadilifu na uwajibikaji ili nao siku moja waondoke kazini kwa heshima kama hiyo.
“Wastaafu hawa wametuachia urithi wa maadili, bidii na busara. Hili ni somo kwetu sote tuliobaki. Tuchukue fursa hii kujitathmini na kujiweka tayari kwa mustakabali wetu,” aliongeza.
Mwisho, aliipongeza Idara ya Elimu Msingi kwa maandalizi mazuri ya hafla hiyo, akisema imefanyika kwa kiwango cha juu na kuonyesha ni kwa namna gani wanathamini watumishi wao.
“Tuna kila sababu ya kuendeleza utamaduni huu wa kuwaaga wenzetu kwa heshima, kwani unajenga mshikamano na kuongeza ari ya utumishi,” alihitimisha.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa