Tarehe 27 Novemba 2025, Halmashauri ya Manispaa ya Geita iliungana na dunia kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia. Maadhimisho haya yalilenga kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kupambana na maambukizi ya VVU, kuimarisha afya ya jamii na kusisitiza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Halmashauri ya Manispaa ya Geita ina jumla ya vituo 10 vya kutolea huduma za tiba na matunzo (CTC) pamoja na vituo 16 vinavyotoa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT). Hadi sasa, jumla ya wateja 10,955 wanaendelea kutumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi ndani ya Manispaa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa, kiwango cha maambukizi ya VVU kimkoa kimefikia asilimia 4.9, ikiwa ni juu kidogo ukilinganisha na wastani wa kitaifa wa asilimia 4.4 Hii inaonyesha uhitaji wa juhudi zaidi katika kuhamasisha upimaji wa hiari, matumizi ya dawa kwa waliogundulika kuwa na maambukizi, na mabadiliko chanya ya mwenendo wa maisha.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Ndugu Yefred Myenzi, aliwataka wananchi kuendelea kutoa elimu juu ya VVU na ukatili wa kijinsia, sambamba na kuweka mipango madhubuti ya maisha ikiwemo kuwekeza, kutunza afya, na kuepuka vitendo visivyofaa. Aidha, alisisitiza viongozi wote kuwa mfano kwa kuepuka matumizi mabaya ya mamlaka dhidi ya watu wanaowaongoza.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa