Mapema leo, 25 Oktoba 2025 Halmashauri ya Manispaa ya Geita kupitia Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Geita Mjini, imeendesha mafunzo ya siku moja kwa makarani waongozaji wa wapiga kura 501, waliopangwa kusimamia vituo 475 vya kupigia kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Katika mafunzo hayo, makarani waliapishwa kwa kula kiapo cha kutunza siri na kujitoa kwenye uanachama wa vyama vya siasa, kama sehemu ya maandalizi rasmi ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa misingi ya uwazi, haki na uaminifu.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Geita Mjini, Ndugu Ndaro Samsoni, aliwapongeza makarani wote kwa kujitokeza kushiriki mafunzo hayo na kuonyesha moyo wa uzalendo. Alisisitiza kuwa nafasi waliyopewa ni ya kuaminiwa, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za uchaguzi.
Aidha, aliwataka kuepuka kutegemea uzoefu pekee na badala yake kuzisoma kwa makini nyaraka zote za uchaguzi, ili kuepuka malalamiko au makosa yanayoweza kudhoofisha uhalali wa mchakato huo muhimu wa kidemokrasia
Katika ujumbe wake wa mwisho, Ndugu Ndaro alieleza kuwa mafanikio ya uchaguzi yanaanza na maandalizi ya makarani, hivyo mafunzo hayo ni msingi imara wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na ufanisi.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa