Katika tukio lenye heshima, uzalendo na shamrashamra za kihistoria, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba (kulia), amekabidhi rasmi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Bi. Grace Kingalame (kushoto), baada ya kukamilika kwa mbio za Mwenge ndani ya Wilaya ya Geita.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 2 Septemba 2025, yakihitimisha safari ya Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri mbili – Halmashauri ya Wilaya ya Geita (Geita DC) na Halmashauri ya Manispaa ya Geita (Geita MC) ambako Mwenge huo umetembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria tukio hilo muhimu ni Ndugu Yefred Myenzi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, ambaye ameungana na viongozi wengine kutoa ushirikiano katika kukamilisha zoezi hilo kwa mafanikio makubwa.
Shughuli hiyo imeonesha mshikamano wa hali ya juu, maandalizi bora, na hamasa kubwa kutoka kwa wananchi na viongozi, wakionesha uzalendo wa dhati kwa kushiriki kikamilifu kwenye mapokezi, mbio, na shughuli zote zilizofanyika.
Halmashauri zote mbili zimepongezwa kwa maandalizi madhubuti, usimamizi mzuri na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua inayoakisi dira ya Taifa la Tanzania katika kuwaletea wananchi wake maendeleo ya kweli.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasomeka:
“Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa Amani na Utulivu”
ujumbe uliobeba dhamira ya kudumisha demokrasia, utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Kwa heri Mwenge wa Uhuru!
Wilaya ya Geita itaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika uzalendo, ushirikiano na utekelezaji wa maendeleo endelevu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa