Leo tarehe 25 Novemba, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Hashim A. Komba amefanya kikao maalum na madereva wa bodaboda na bajaji kutoka maegesho yote ya Kata ya Nyankumbu, ambapo ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kuwawezesha vijana hao kupata leseni kwa gharama nafuu na muda mfupi zaidi.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya alieleza kuwa bado kuna changamoto kadhaa katika upatikanaji wa leseni ikiwemo:
1. Gharama kubwa za kulipia chuo cha mafunzo,
2. Muda mrefu wa mafunzo, ambapo ilibainika kuwa elimu hiyo imekuwa ikichukua hadi mwezi mmoja, jambo linalowakwamisha vijana wanaotegemea kazi hizo kwa kipato cha kila siku,
3. Gharama ya leseni yenyewe, ambayo serikali tayari imeifanyia kazi kwa kupunguza bei.
Amesema kama wilaya wamefanya mazungumzo na Chuo na kuweka mipango madhubuti kwa kupunguza muda wa mafunzo kutoka siku 30 hadi siku 3, pamoja na gharama ya leseni na mafunzo kutoka viwango vya awali hadi Shilingi 85,000.
Aidha, amezitaka Halmashauri za Wilaya Geita kuandaa programu maalum ya kutumia asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha vijana wasiokuwa na leseni kupitia mfumo wa mikopo nafuu. Katika mpango huo, halmashauri italipia gharama za mafunzo na leseni kwa vijana, na kila mmoja atalipa mkopo huo kwa kipindi cha miezi 12, bila riba.
Amesema njia hiyo ni bora zaidi kuliko kuwakopesha pikipiki au bajaji kabla hawajapata leseni, kwani inalenga kuwajengea uwezo wa kisheria na usalama barabarani.
Katika hitimisho la kikao hicho, Mkuu wa Wilaya amewasihi vijana hao kuendelea kulinda amani na utulivu wa Geita na Taifa kwa ujumla, huku akiwataka kuachana na vitendo visivyofaa na kuwa mabalozi wa nidhamu, uadilifu na uwajibikaji.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa