Kikao cha tathmini ya kampeni ya usafi wa mazingira katika Wilaya ya Geita chenye kauli mbiu “HYAGULAGA GEITA” kimefanyika leo kwa mafanikio makubwa, kikihusisha wadau mbalimbali wa usafi wa mazingira, watendaji wa kata, vijiji na mitaa.
Kikao hicho kiliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim A. Komba, Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Komba aliipongeza jamii ya Geita kwa ushiriki mkubwa kwenye kampeni ya usafi na akatoa tuzo kwa mitaa iliyofanya vizuri.
Washindi wa Kampeni ya Usafi:
- Mtaa wa Shilabela – Tsh 1,000,000/=
- Mtaa wa Nyerere Road – Tsh 600,000/=
- Mtaa wa Upendo – Tsh 400,000/=
Kwa upande mwingine, mitaa iliyofanya vibaya katika suala la usafi imekabidhiwa bendera nyeusi kama ishara ya tahadhari, ambapo mitaa hiyo ni:
- Nyantorontoro A
- Uwanja
- Tambuka Reli
Mhe. Komba amesisitiza umuhimu wa kuendeleza kampeni hii kila mtaa, kwa kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora na mji unakuwa safi Amesema kuwa kutakuwa na zawadi zaidi kwa washindi na kamati maalum za usafi zitaanzishwa ili kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Katika hotuba yake, Mhe. Komba pia aligusia changamoto ya utozaji wa faini kwa wafanyabiashara wadogo, akisema:
“Wananchi wengi hawana elimu juu ya usafi. Badala ya kuwatoza faini, tuwape elimu. Wafanyabiashara wadogo wana mitaji midogo, faini inawavunja moyo. Tuwahurumie, tusijipatie laana kwa Mwenyezi Mungu.”
Watendaji wa mitaa, viongozi wa vijiji, na wananchi waliotoa maoni mbalimbali wamehimiza uboreshaji wa elimu ya usafi, usimamizi thabiti, na ushirikiano wa jamii katika kuendeleza kampeni ya HYAGULAGA GEITA kwa mafanikio ya pamoja.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa