Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Bi. Lucy Beda, amefungua rasmi mafunzo kwa wanachama wa vikundi vilivyoidhinishwa kupokea mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Geita kwa dirisha la Julai – Septemba 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Lucy Beda amepongeza vikundi vilivyokidhi vigezo vya kupata mkopo huo, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyopangwa. Ameonya dhidi ya mwelekeo wa baadhi ya vikundi kufanya shughuli nje ya maandiko yao, jambo linalohatarisha urejeshaji wa mikopo na kuwanyima wengine fursa hiyo muhimu.
Aidha, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita Ndugu Yefred Myenzi kwa Ukusanyaji na usimamizi thabiti wa mapato yanayo wezesha Kutenga asilimia 10 kwaajili ya Mikopo hiyo, pamoja na Idara ya Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Ndugu Robert Sungura, kwa namna wanavyosimamia vikundi na kutoa elimu endelevu kwa wanufaika.
Amesema ili mikopo iwe na tija, wanavikundi wanapaswa kuwa na fikra za miradi mikubwa.
“Tuvuke hatua ya kukopa milioni tatu, tuanze kufikiria miradi ya milioni 100,” alisema Bi Lucy.
Kwa upande wake, Ndugu Robert Sungura Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Geita amesema mafunzo hayo yatasaidia vikundi kuelewa namna bora ya kuendesha miradi na kujenga msingi imara wa marejesho. Ameeleza kuwa elimu hiyo itatolewa katika kila kata ili kuwafikia wanavikundi wote.
Katika dirisha hili, vikundi 123 ni vya wanawake, 101 vya vijana na 7 vya watu wenye ulemavu.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa