Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashim Komba amekabidhi hundi ya mfano ya Shilingi Bilioni 2.99 kwa vikundi 231 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Geita.
Hafla hii ya utoaji mikopo imefanyika leo Novemba 19, 2025 katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo katika Kata ya Bombambili na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wanufaika wa mikopo hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo, Mhe. Komba ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyokuwa na riba.
Aidha, amewataka wanufaika kuhakikisha fedha hizo zinatumika katika shughuli za kiuchumi na sio kwa matumizi yasiyo na tija, huku akisisitiza ulazima wa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili wengine waweze kunufaika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Ndg. Yefred Myenzi, amesema kwa awamu hii Manispaa ilitenga Bilioni 3.1 na vikundi vyote vilivyoomba mikopo na vyenye sifa vimeweza kupatiwa kiasi cha Bilioni 2.99 na vile ambavyo havikuwa na sifa vimeelekezwa kuboresha changamoto zilizopo ili awamu inayofata viweze kuomba vikiwa na sifa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mikopo ya asilimia 10 ngazi ya Wilaya, Bi. Lucy Beda, amesema vikundi vyote vilivyopata mikopo vilikidhi vigezo na vimepatiwa elimu ya ujasiriamali na namna bora ya kutumia na kurejesha mikopo hiyo na zoezi hilo linaendelea kwa awamu ili kuhakikisha makundi mengi zaidi yanahusishwa.
Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa, Afisa Maendeleo ya Jamii, Bi. Mariam John amesema Vikundi vya Wanawake 123 vimepata mkopo wa shilingi 1,168,500,000/=, Vikundi vya Vijana 101 vimepata mkopo wa shilingi 1,785,000,000/= na Vikundi vya watu wenye Ulemavu 7 vimepata mkopo wa shilingi 44,000,000/=.
Geita Tanzania
Sanduku la Posta: P.o Box 384 Geita
Namba ya Simu: 0282520437
Mobile:
Barua pepe: td@geitatc.go.tz
Hatimiliki 2017 Halmashauri ya Mji Geita . Haki zote zimehifadhiwa